ZAKA ZA FITRI NA SWALA YA IDDI KATIKA UISLAMU

Allah (Subhaanahu wa Taala) ametuwekea zaka za fitri kwa hikma ya kuwa ni kafara pindi unapopatikana upungufu katika saumu ya Muislamu katika Mwezi wa Ramadhani. Na hakika hakuna binadamu mkamilifu. Na Iddi imewekwa ili kuonyesha kuwa Uislamu unazingatia maumbile ya binadamu, kwani binadamu huwa anapenda kuwa na wakati wa kusherehekea, kwa ajili hiyo ndio ikawekwa Iddi mbili ili ziwe sherehe zetu zimefungamana na ibada.

Kubainisha Maana ya Zaka za Fitri na Hukumu yake.

Ni nini maana ya zaka za fitri? Kabla ya kueleza hilo, napenda kuwakumbusha waja wa Allah ya kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mgeni mtukufu aliyetujilia na amekurubia kuondoka. Inatakikana tupatilize siku zillizobakia kwa wingi wa toba na amali njema huenda Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) akaziunganisha amali zetu.

Enyi waja wa Allah, Mwisho wa mwezi huu mtukufu kuna amali tukufu zenye kuzidisha imani na kukamilisha ibada zetu, na amali hizo ni; zakatul fitri, takbira na swala ya iddi. Na zakatul fitri ni sadaka ambayo inapasa kwa sababu ya kufungua mwezi wa Ramadhani, na hakika imetambuliwa zaka za fitri kuwa ni swadaka ya wajibu, kwa hivyo ndio tunaiita zaka za fitri sadakatul fitri. Sasa twende katika kueleza hukumu ya zaka za fitri na dalili ya kuwekwa ibada hii.

Wanazuoni wa fiq’hi wameafikiana ya kuwa zaka za fitri inampasa kila Muislamu mwenye uwezo. Na dalili ni hadithi iliyopokewa na Ibnu ‘Umar asema katika mafhuum ya maneno yake: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amefaradhishia watu inapomalizika Ramadhani kutoa pishi ya tende au pishi ya ngano, na hilo ni kwa kila Muislamu, awe muungwana au mtumwa, mume au mke”. Amepokea hadithi hii Bukhari.

Hikma ya kuwekwa Zaka za Fitri

Ni muhimu Muislamu kujua hikma ya zaka za fitri, hikma ya zaka za fitri ni mambo mawili :-


Hikma ya kwanza ni kuwa inatwahirisha saumu ya mwenye kufunga. Kwani binadamu kwa ubinadamu wake anaweza kufanya mambo ya kumpunguzia thawabu, basi hapo ndipo inapokuja nafasi ya zaka za fitri. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ametuambia katika hadithi iliyopokewa na Ibnu ‘Abbas katika maana ya hadithi: [Zaka za fitri ni twahara ya mwenye kufunga kutokana na upuuzi na maneno machafu, na ni chakula kuwalisha maskini]. Imepokewa na Abu Daud.

Hikma ya pili ni kuwakunjua mafukara na maskini na kuingiza furaha nyoyoni mwao.